Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

HOTUBA YA MHESHIMIWA ATUPELE FREDY MWAKIBETE (MB), NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (SEKTA YA UCHUKUZI) KWENYE UFUNGUZI WA HAFLA YA UTOAJI WA VYETI KWA MADEREVA WALIOTHIBITISHWA NA LATRA
01 Jul, 2023 Pakua
  • CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA,
  • SACP. Ramadhani Ng’anzi, Kamanda wa Polisi - Kikosi cha Usalama Barabarani,
  • Dkt. Zainab Rashid, Mwenyekiti wa Kamati ya Uthibitishaji Madereva-LATRA
  • Ndugu Viongozi na wawakilishi wa Taasisi za Serikali mliopo hapa,
  • Ndugu Wenyeviti na Viongozi wa Vyama vya Madereva na Wasafirishaji ikiwemo CHAWAMATA, TADWU, UWAMATA, TATOA, TAT, TAMSTOA, TRFA, DARCOBOA  NA UWADAR,  
  • Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa
  • Ndugu wanahabari,
  • Wageni waalikwa mabibi na mabwana, Itifaki imezingatiwa,

Nawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…

Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi MUNGU mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai, afya na kuibariki Serikali yetu ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Pili, naishukuru sana Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii muhimu ya utoaji wa vyeti kwa madereva wa vyombo vya moto vinavyotoa huduma ya usafiri kibiashara waliofanya mtihani na kuthibitishwa na LATRA pamoja na kuzindua mitaala ya mafunzo ya wahudumu wa vyombo hivyo.

 

Kwa hakika, leo ni siku muhimu sana katika historia ya Nchi yetu na hususan Sekta ya Uchukuzi na Mdhibiti (LATRA) kwa kuweza kutekeleza kifungu cha 5(1)(e) ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413 iliyopitishwa na Bunge la Tanzania Mwaka 2019 na Kanuni za Usajili wa Wahudumu na Uthibitishaji wa Madereva ya Mwaka 2020. Historia hii inaandikwa na kundi hili la kwanza la madereva takriban 1,000 waliothibitishwa na Mdhibiti ambapo leo tunawakabidhi vyeti vya kuthibitishwa na Mamlaka. Vyeti hivi vitatambulika kitaifa na kimataifa kwa na hasa kwa Nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Kabla ya sijaendelea na maudhui ya hotuba yangu, naomba niseme machache kuhusu Uongozi mahiri wa Awamu ya Sita. Sote ni mashahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inafanya juhudi kubwa na za kupigiwa mfano kimataifa katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuhakikisha matukio ya ajali yanapungua sana nchini kama sio kumalizika kabisa. Rais wetu mpendwa anatambua kuwa kupitia ajali, nchi imekuwa ikipoteza nguvukazi ya Taifa pamoja na mali, huku baadhi wakiachwa bila wazazi na wengine kupata ulemavu wa maisha unaowanyima fursa ya kufanya shughuli zao vyema nap engine wanakuwa tegemezi kwa jamii. Jambo hili linamnyima usingizi Rais wetu na ndio maana anafanya kila linalowezekana kuhakikisha matukio ya ajali zinazogharimu Nchi yetu yanapungua au hata kwisha kabisa.

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Ninatambua kwamba takwimu duniani zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 76 ya ajali zinazotokea barabarani zinasababishwa na makosa ya kibinadamu. Naomba nichukue fursa hii kulipongeza Bunge la Tanzania kwa kutunga Sheria iliyoipa LATRA jukumu la kuthibitisha madereva wa vyombo vya usafiri kibiashara. Niwapongeze pia LATRA kwa kutekeleza Sheria hiyo na kuweza kuweka utaratibu wa kuthibitishaji madereva hao.

 

Aidha, nawapongeza sana LATRA kwa kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo Jeshi la Polisi,  Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na VETA kwa kuandaa kwa pamoja maswali yenye nia njema ya kufahamu uelewa wa madereva wetu.

 

Vilevile, nawapongeza sana madereva wote waliojitokeza na kufanya mitihani hii. Ninaamini hata wale ambao hawakufaulu, wamejikumbusha mambo kadhaa na niwasihi wasikate tamaa bali wajikumbushe tena yale waliyojifunza na warudi kufanya mitihani hii ili wathibitishwe na tuje kuwapatia vyeti siku chache zijazo. Nawashukuru pia wamiliki wa vyombo waliowapa madereva wao fursa ya kushiriki mitihani hii na wote waliowezesha mafanikio yaliyopatikana hadi hatua hii. Nimejulishwa kuwa kuna baadhi ya kampuni na wasafirishaji wamekuwa mstari wa mbele kuwawezesha madereva wao kujisajili na kufanya mtihani wa LATRA ili wathibitishwe. Hili ni jambo jema sana na nitafurahi LATRA ikiweka utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza makampuni yenye idadi kubwa ya madereva waliothibitishwa na LATRA. Naelekeza mwakani katika kuadhimisha wiki ya usalama barabarani, ufanyike utaratibu wa Mgeni Rasmi, pengine Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa tuzo kwa kampuni itakayoongoza kuwa na idadi kubwa na kutosababisha ajali barabarani kwa kila mwaka.

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Juhudi hizi za LATRA kwa kushirikiana na ninyi wadau (madereva na waajiri wenu) haziendi bure bali zinaenda kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri ardhini hapa nchini kwa kuwa yataleta mabadiliko ya tabia za madereva wakiwa barabarani na bila shaka tutaona tofauti ya dereva aliyethibitishwa na LATRA na yule ambaye hakuthibitishwa na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa sekta ya usafirishaji.

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Suala hili la uthibitishaji wa madereva linalofanywa na LATRA lina faida nyingi ikiwemo kupata kumbukumbu ya mwenendo wa dereva katika kazi hasa Kampuni alizopitia, kuwezesha wamiliki wa magari kuwa na madereva wenye weledi na nidhamu, kusaidia upatikanaji wa madereva mahiri, kusaidia madereva kujikumbusha mambo waliyosoma darasani, kuwawezesha madereva kutambulika na kupatiwa mikataba ya ajira na kuitangaza Nchi yetu duniani kwa namna madereva wanavyokuwa weledi.

 

Faida nyingine ni kwamba, inawaongezea imani abiria wanaotumia vyombo vya usafiri kwamba wanaendeshwa na madereva waliothibitishwa uwezo wao, inawaongezea imani wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa vyombo vyao vinaendeshwa na madereva mahiri waliothibitishwa na Mamlaka halali ya Serikali na itawapa fursa za ajira ya udereva nje ya Tanzania. Serikali inaamini kuwa hadhi ya madereva itaongezeka, wataheshimika zaidi na maslahi yao yataboreshwa na zaidi, taaluma hii ya udereva itarasimishwa na kuwaongezea madereva thamani kwenye masoko ya ajira ya ndani na nje ya nchi, hususan kwenye nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Kutokana na faida hizo, kipekee niwapongeze sana madereva waliofanya mtihani na kufaulu. Lakini pia niwatie moyo wale ambao hawakufanya vizuri wajiandae na mtihani huo. Mkurugenzi Mkuu LATRA, CPA Habibu Suluo, kwenye hotuba yake ameeleza kuwa zipo video zilizoandaliwa ambazo zitawasaidia katika maandalizi ya mtihani huu. Kwa hiyo tumieni muda wenu wa ziada kuzitazama, kujikumbusha na kujifunza ili unapoingia kwenye chumba cha mtihani uwe na uelewa wa masuala kadha wa kadha. Lakini pia, nitoe rai kwa madereva ambao bado hawajajisajili kwa ajili ya kuthibitishwa, wafanye hivyo kabla ya tarehe 31 Julai, 2023. 

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Kwa upande wetu, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Sekta ya Uchukuzi itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuiwezesha LATRA kutekeleza jukumu hili ambalo ni muhimu na kwa mujibu wa sheria.

 

Nawasihi wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi hizi za Serikali ukizingatia ukweli kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za usafirishaji kwa kushirikiana na sekta binafsi.

 

Ndugu Viongozi, Madereva na Wageni waalikwa,

Kwa hayo machache, napenda kutamka kuwa nimefungua rasmi hafla hii na sasa nipo tayari kwa ajili ya jukumu la Uzinduzi wa Mitaala itakayotumika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa magari ya kibiashara pamoja na kutoa  vyeti kwa madereva waliofanya mtihani na kuthibitishwa na LATRA.

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

 

Atupele Fredy Mwakibete (Mb)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (SEKTA YA UCHUKUZI)

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo