Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

LATRA YADHAMINI WAHUDUMU 10 WA VYOMBO VYA MOTO KIBIASHARA
Imewekwa: 22 Nov, 2023
LATRA YADHAMINI WAHUDUMU 10 WA VYOMBO VYA MOTO KIBIASHARA

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imedhamini kwa kulipa ada za mafunzo kwa wahudumu 10 wa vyombo vya moto kibiashara kutoka kwa kampuni 10 za mwanzo zilizowasilisha orodha ya wahudumu/makondakta waliokuwa tayari kuanza mafunzo yatakayotolewa na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) pamoja na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Hayo yamebainishwa na CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mafunzo ya wahudumu/makondakta wa vyombo vya moto kibiashara iliyofanyika Novemba 22, 2023 katika ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam.

CPA Suluo amesema kuwa, wahudumu watano watapatiwa mafunzo hayo Chuo cha NIT na wengine watano chuo cha CBE na amewasihi wahudumu hao kuzingatia mafunzo ili kuongeza tija wanapotekeleza majukumu yao ya kuwahudumia abiria.

“Ninawasihi wahudumu/makondakta kuzingatia masomo yenu, msome kwa bidii na baada ya kufaulu mfike LATRA kwa ajili ya kusajiliwa.  Usajili utafanyika kupitia mfumo wetu wa kidigiti (rrims.latra.go.tz) na kila muombaji atatakiwa kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA), Cheti cha mafunzo kutoka CBE au NIT na Cheti cha Uchunguzi wa Afya ili aweze kusajiliwa,” ameeleza CPA Suluo.

Aidha, CPA Suluo ameongeza kuwa, mkazo wa mafunzo hayo utawekwa kwenye kufahamu Sheria, Taratibu, Kanuni na Kujali Wateja (Customer Care), na Kanuni itayosisitizwa ni ile inayohusu Usajili wa Wahudumu ili wajue majukumu yao na pale wasipoyapotimiza wafahamu wanatenda kosa lenye kustahili adhabu.

CPA Suluo amezitaja faida za wahudumu wa vyombo vya moto kibiashara kuhudhuria mafunzo na kisha kusajiliwa na Mamlaka ambazo ni, Wamiliki kupata wasimamizi mahiri na weledi wa kazi waliyopewa, Wahudumu kufanya kazi kwa weledi, umakini na ufanisi zaidi, Kuboresha huduma za usafiri ardhini hususana wa abiria nchini, Abiria kuvutiwa na huduma nzuri inayotolewa na kupata amani safarini, Kurasimisha kazi ya wahudumu iheshimike kama zilivyo kazi nyingine, Kulinda mitaji ya wamiliki wa vyombo na vipato vya wahudumu, Kuwezesha taasisi zinazoshughulikia masuala ya ajira kuwa na taarifa sahihi zinazowezesha kusimamia maslahi ya wahudumu katika ajira na Kuongeza nidhamu na uwajibikaji kwa wahudumu na watumiaji wa huduma.

Naye Bw. Priscus Joseph, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), amesema mafunzo hayo kwa wahudumu yanaenda kuboresha utoaji wa huduma kwa kuwa yanaenda kuongeza weledi na tija. Pia amewasihi wahudumu hao kuwakumbusha abiria ishara za kiusalama ndani ya mabasi, wawe karibu na madereva na kuwakumbusha kutoendesha chombo cha moto kwa mwendokasi pamoja na kuwakumbusha abiria kutokuwa na haraka ya kufika ili dereva aweze kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo pindi anapokuwa safarini.

Nao wakufunzi kutoka Chuo cha CBE na NIT wameishukuru LATRA kwa kuwashirikisha katika mchakato mzima wa uandaaji wa mtaala na uzinduzi wa mafunzo hayo na wamesema, “Tumejipanga vizuri kuwapatia mafunzo na tutatumia umahiri wetu na uzoefu tulionao katika kutoa mafunzo haya kwa wahudumu, ili kuhakikisha wanakuwa bora wanapotekeleza majukumu yao na kuifanya sekta ya usafiri ardhini kuwa yenye tija.”

Mafunzo ya wahudumu/makondakta wa vyombo vinavyotoa huduma za usafiri kibiashara yatatolewa kwa kuzingatia mitaala ya CBE na NIT iliyozinduliwa rasmi na Mhe. Atupele Freddy Mwakibete aliyekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, tarehe 1 Julai, 2023.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo