Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Uchukuzi

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini

Piga Bure : 0800110019/0800110020
LATRA Logo

MABASI 36, MADEREVA 10 WAFUNGIWA KWA KUKIUKA MASHARTI YA LESENI
Imewekwa: 10 Nov, 2023
MABASI 36, MADEREVA 10 WAFUNGIWA KWA KUKIUKA MASHARTI YA LESENI

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha leseni za mabasi 36 kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo kuingilia Mfumo wa Kufuatilia Mwenendo wa Magari (VTS) na kupelekea mwendokasi hatarishi kinyume na Sheria za Usalama barabarani. kufuatia tathmini iliyofanyika ya mabasi hayo yanayofanya safari za masafa marefu kwa saa 24.

Hayo yamesemwa na CPA Habibu Suluo, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA wakati Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ukumbi wa mikutano ofisi ya LATRA Mkoa wa Dar es Salaam Novemba 9, 2023 kuhusu tathmini ya mabasi yaliyopewa ratiba za safari za usiku kuanzia Oktoba mosi mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari CPA Suluo amesema kuwa asilimia kubwa ya mabasi yaliyopewa ratiba za kufanya safari usiku yanakiuka Sheria za Usalama Barabarani na Masharti ya Leseni zao, hivyo imepelekea Mamlaka kuchukua hatua.

“Kufuatia tathmini ya safari za saa 24 tumebaini kati ya mabasi 246 ambayo yamepewa ratiba za kufanya safari za usiku, 80% ya mabasi hayo (Mabasi 197) yanaendeshwa mwendo hatarishi kati ya kilomita 86-89 kwa saa, na 09% ya mabasi yo yanaendeshwa mwendo hatarishi zaidi kati ya kilomita 90-103 kwa saa, hivyo LATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tumechukua hatua yakusitisha leseni za Mabasi 36 mpaka Mamlaka itakapo jiridhisha kuwa kampuni hizo zimejirekebisha” Amesema CPA Suluo.

Aliongeza kuwa, tathmini hiyo imeonesha kuna baadhi ya wasafirishaji hawatekelezi utaratibu ulioelekezwa na Kanuni za leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria kutumia madereva wawili kwa safari za njia ndefu zinazozidi kilomita 700, ambapo baadhi ya madereva huepuka matumizi ya kitufe cha utambulisho (I- Botton) ambacho ni muhimu ili kuiwezesha Mamlaka kumtambua dereva na muda aliokuwa anaendesha gari husika.

“Katika ufuatiliaji wetu, tumebaini baadhi ya madereva wanafanya safari ndefu bila kuwa na dereva wa pili, na kuna madereva wanafika saa nne usiku, wanapumzika kwa saa chache na kuanza safari nyingine usiku huo huo” Alisema

Aidha, CPA Suluo alisema kuwa ni lazima wamiliki wa mabasi wahakikishe wanatoa tiketi za kielektroni zenye taarifa za msingi na sahihi za abiria ili kuhakikisha kila abiria anayesafiri anatambulika na kumuwezesha kupata haki zake endapo atakumbana na kadhia yeyote.

“Suala la kuandika taarifa za msingi na sahihi za abiria ni la lazima, na sio tu kwa wanaofanya safari za usiku, hii inawagusa wote, na haitakiwi taarifa hizi ziandikwe kwa mkono, tunaelekea kusaini Mkataba wa Maelewano (MOU) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) ili kuwasaidia wananchi kupata stahiki zao wanapopata ajali, bila ya taarifa hizi itakuwa ngumu kufanikisha hilo” Ameongezea CPA Suluo.

Kwaupande wake SACP Ramadhan Ng’anzi, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani ametangaza kufungiwa leseni za madereva 10 ambao wamebainika kukiuka Sheria za Usalama Barabarani na kuhatarisha maisha ya abiria na mali zao na kuwa baada ya kutumikia kifungo cha leseni zao hawatarejeshewa leseni hizo hadi watakapofuata utaratibu wa kusailiwa na kupata leseni.

“Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limefungia leseni za maderva 10 na hawataruhusiwa kuendesha gari lolote kwa kipindi chote cha kutumikia adhabu, hatutovumilia madereva wanaokiuka Sheria, kwa kushirikiana na Mamlaka tumefungia leseni za madereva hao na wengine kufikishwa mahakani pamoja na kufutiwa leseni kwa kosa la kuingilia Mfumo wa VTS na kwenda mwendo kasi unao hatarisha maisha ya binadamu na mali zao” Amesema SACP Ng’anzi.

Naye Bw. Priscus Joseph, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) amewaasa madereva na wamiliki kufuata Sheria za Usalama Barabarani pamoja na Masharti ya leseni zao huku akiiomba LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kukishirikisha chama hicho wakati wa kuchukua hatua.

“Niwasihi tu madereva na wamiliki wenzangu wa abasi tuendeshe kwa mwendo unaotakiwa, hata kwa mwendo chini ya kilomita 80 kwa saa hasa katika kipindi hiki cha mvua, hata hivyo siku hizi tuna hadi safari za usiku hivyo sioni sababu itakayotufanya tushindane. Hivyo, tuendelee kutii Sheria, pia naiomba LATRA kutushirikisha juu ya taarifa ya kufungia mabasi kabla ya kuchukua hatua za kisheria.” Amesema Bw. Joseph.

Kwa upande wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC)  limeishukuru LATRA na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kusimamia vyema usalama wa usafiri ardhini na limewashauri watoa huduma wa usafiri kuzingatia usalama wa abiria, na usalama wa vyombo vya usafiri ili kuwezesha huduma za Usafiri kuwa endelevu.

 

Mrejesho

Mrejesho, Malalamiko au Wazo